Jeremiah 18

Katika Nyumba Ya Mfinyanzi

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana: 2“Shuka uende mpaka nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.” 3Kwa hiyo nikashuka mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake. 4Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake, hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kama vile ilivyoonekana vyema kwake yeye.

5Kisha neno la Bwana likanijia kusema: 6 a“Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” asema Bwana. “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli. 7 bIkiwa wakati wowote nikitangaza kuwa taifa au ufalme utang’olewa, utaangushwa na kuangamizwa, 8 cikiwa lile taifa nililolionya litatubia uovu wake, ndipo nitakapokuwa na huruma, wala sitawapiga kwa maafa niliyokuwa nimewakusudia. 9 dIkiwa wakati mwingine nitatangaza kuwa taifa ama utawala ujengwe na kuwekwa wakfu, 10 eikiwa utafanya maovu mbele zangu na hukunitii, ndipo nitakapoghairi makusudio yangu mema niliyokuwa nimeyakusudia.

11 f“Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Tazama! Ninaandaa maafa kwa ajili yenu, nami ninabuni mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka njia zenu mbaya, kila mmoja wenu, tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’ 12 gLakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’ ”

13 hKwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana: “Ulizia miongoni mwa mataifa:
Ni nani alishasikia jambo kama hili?
Jambo la kutisha sana limefanywa
na Bikira Israeli.

14 Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka
kwenye miteremko yake ya mawe wakati wowote?
Je, maji yake baridi yatokayo katika vyanzo vilivyo mbali
yaliwahi kukoma kutiririka wakati wowote?

15 iLakini watu wangu wamenisahau mimi,
wanafukizia uvumba sanamu zisizofaa kitu,
zilizowafanya wajikwae katika njia zao
na katika mapito ya zamani.
Zimewafanya wapite kwenye vichochoro
na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.

16 jNchi yao itaharibiwa,
itakuwa kitu cha kudharauliwa daima;
wote wapitao karibu nayo watashangaa
na kutikisa vichwa vyao.

17 kKama upepo utokao mashariki,
nitawatawanya mbele ya adui zao;
nitawapa kisogo wala sio uso,
katika siku ya maafa yao.”

18 lWakasema, “Njooni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njooni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali chochote asemacho.”
19 Nisikilize, Ee Bwana,
sikia wanayosema washtaki wangu!

20 mJe, mema yalipwe kwa mabaya?
Lakini wao wamenichimbia shimo.
Kumbuka kwamba nilisimama mbele yako
na kunena mema kwa ajili yao,
ili wewe ugeuze hasira yako kali mbali nao.

21 nKwa hiyo uwaache watoto wao waone njaa;
uwaache wauawe kwa makali ya upanga.
Wake zao wasiwe na watoto, na wawe wajane;
waume wao wauawe,
nao vijana wao waume
wachinjwe kwa upanga vitani.

22 oKilio na kisikike kutoka kwenye nyumba zao
ghafula uwaletapo adui dhidi yao,
kwa kuwa wamechimba shimo ili kunikamata
na wameitegea miguu yangu mitego.

23 pLakini unajua, Ee Bwana,
hila zao zote za kuniua.
Usiyasamehe makosa yao
wala usifute dhambi zao
mbele za macho yako.
Wao na waangamizwe mbele zako;
uwashughulikie wakati wa hasira yako.
Copyright information for SwhKC